emblem

The United Republic of Tanzania

Tanzania Civil Aviation Authority-Consumer Consultative Council (TCAA-CCC)

News

ENDELEENI KUSIMAMIA NA KUWAWAKILISHA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA ANGA - NAIBU WAZIRI


Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (MB) amelipongeza Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA-CCC) kwa kuendelea kusimamia na kuwawakilisha watumiaji wa huduma anga nchini.

Mhe. Kihenzile amesema hayo baada ya kutembeleza ofisi za Baraza katika ziara yake rasmi ya kikazi jijini Dar es Salaam.

"Baraza limeendelea kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma ya usafiri wa anga kwa kutoa taarifa na maoni muhimu kuhusu masuala mbalimbali kwenye usafiri wa anga", alisema Mh. Kihenzile na kuongeza;

"Pamoja na uchache wenu mmejitahidi kuwafikia wadau wengi ambapo kati ya maoni na malalamiko yaliyowasilishwa hadi sasa, asilimia 89 yameshafanyiwa kazi kwa ukamilifu wake".

Mhe. Kihenzile alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya maboresho muhimu katika viwanja vya ndege ikiwemo kujenga na kuboresha viwanja vya ndege (Mbeya, Rukwa, Lindi, Mtwara, Kigoma, Njombe, Musoma na Iringa), na kufanya upanuzi wa majengo ya abiria (Arusha, Kahama, Ruvuma).

"Maboresho haya yatavutia makampuni mengi zaidi yanayotoa huduma za usafiri wa anga na kuongeza ushindani sokoni. Hivyo nawaagiza Baraza kuboresha mikakati yake ili tupokee maoni mengi juu ya huduma zetu", alisema Mhe. Kihenzile na kuongeza kuwa dhumuni la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kituo namba moja kwa utoaji wa huduma bora za anga barani Afrika.

Katibu Mtendaji wa TCAA-CCC, Bw. Innocent Kyara alisema Baraza litaendelea kutoa elimu kwa wadau wote ili kuhakikisha maslahi ya watumiaji wa huduma za anga yanalindwa.

"Tutaendelea kutoa elimu kwa kutumia vyombo vya habari, mafunzo, maonesho, mitandao ya kijamii na mikutano ya wadau ili kuhakikisha haki na wajibu wa mtumiaji wa huduma za anga vinazingatiwa", alisema Bw. Kyara.

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA-CCC) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 56 cha Sheria ya Usafiri wa Anga, Sura ya 80 Toleo la mwaka 2020 kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za usafiri wa anga.