emblem

The United Republic of Tanzania

Tanzania Civil Aviation Authority-Consumer Consultative Council (TCAA-CCC)

News

TANGAZO LA NAFASI ZA WAJUMBE WA BARAZA LA USHAURI LA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA (TCAA-CCC)


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI TANGAZO LA NAFASI ZA WAJUMBE WA BARAZA LA USHAURI LA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA (TCAA-CCC)

1. UTANGULIZI

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA-CCC) limeundwa chini ya Kifungu cha 56(2) cha Sheria ya Usafiri wa Anga Sura ya 80 Toleo la Mwaka 2020. Baraza lina wajibu wa kutetea na kuwakilisha maslahi ya watumiaji wa huduma za usafiri zinazodhibitiwa na TCAA. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Waziri mwenye dhamana na masuala ya Uchukuzi amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe wa Baraza kutoka miongoni mwa wadau au watumiaji wa huduma za usafiri wa Anga wenye sifa za kujaza nafasi hizo. Ili kuwezesha uteuzi huo, Katibu Mkuu anakaribisha maombi kutoka kwa Watanzania wenye sifa na uwezo wa kujaza nafasi za Wajumbe wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Anga kama ilivyoainishwa katika tangazo hili.

2. KAZI ZA BARAZA LA USHAURI LA WATUMIAJI HUDUMA ZA USAFIRI WA ANGA

Kwa mujibu wa Kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Usafiri wa Anga majukumu ya Baraza ni pamoja na:-

(a) Kuwakilisha maslahi ya watumiaji kwa kufanya mawasilisho, kutoa maoni na taarifa na kushauriana na TCAA, Waziri pamoja na Mawaziri wa Sekta nyingine zinazodhibitiwa na TCAA

(b) Kupokea na kusambaza taarifa na maoni kuhusiana na mambo yenye maslahi kwa watumiaji wa huduma na bidhaa zinazodhibitiwa na TCAA;

(c) Kuunda Kamati za Watumiaji wa Huduma za usafiri wa Anga za Mikoa na za Kisekta zinazodhibitiwa na TCAA na kushauriana na Kamati hizo; na

(d) Kufanya utafiti juu ya mambo yanayoathiri maslahi ya Watumiaji wa Sekta inayodhibitiwa na TCAA.

3. SIFA ZA WAOMBAJI

Kwa mujibu wa Kifungu cha 56(4) cha Sheria ya Usafiri wa Anga, Uteuzi wa Wajumbe wa Baraza utazingatia watu waliohitimu Kidato cha Nne/Sita waliofuzu Shahada/Stashahada ya Juu na wenye uelewa wa kutosha juu ya maslahi ya wa huduma zinazodhibitiwa na TCAA ikiwa ni pamoja na maslahi ya:- (a) Watu wenye kipato cha chini; (b) Jumuia za wenye viwanda na wafanyabiashara; (c) Serikali na mashirika ya kijamii.

4. JINSI YA KUTUMA MAOMBI

Maombi yote yaambatishwe na taarifa binafsi (CV), nakala za vyeti vya taaluma, picha ndogo ya rangi (passport size) ya hivi karibuni pamoja na majina ya wadhamini watatu (3) yakiwa na anuani kamili, barua pepe na namba zao za simu.

Maombi yawasilishwe kwa anuani ifuatayo:-

Katibu Mkuu,

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi),

Mji wa Serikali Mtumba,Mtaa wa Ujenzi,

S.L.P. 638, DODOMA

Mwisho wa Kupokea Maombi ni tarehe 1 Juni, 2023. Tangazo hili limetolewa na:- Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mji wa Serikali Mtumba, Mtaa wa Ujenzi, S.L.P. 638, DODOMA